Mwanamke ni Tishio: Jinsi ya Kutambua Nguvu Yako ya Kiroho katika Ufalme wa Mungu
![]() |
| The Woman is a Threat: Unlock your true identity to protect your family and rule with divine wisdom. _GDBxhop |
MWANAMKE NI TISHIO:
Jinsi ya Kutambua Nguvu Yako ya Kiroho katika Ufalme wa Mungu
Utangulizi
Bwana Yesu asifiwe sana mtu wa Mungu! Ni heshima kubwa kukukaribisha katika makala hii ya kipekee. Katika ulimwengu wa roho, kuna ukweli mmoja ambao adui anajaribu kuuficha: Mwanamke anapojitambua, anakuwa "bomu la nyukilia" dhidi ya ufalme wa giza.
Andiko letu kuu katika makala hii ni:
"Bwana Mungu akasema, 'Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.'" (Mwanzo 2:18).
Wengi wameelewa vibaya neno "msaidizi" (Ezer), wakilichukulia kama alama ya udhaifu. Lakini kiukweli, katika lugha ya awali, neno hili linabeba dhana ya nguvu ya ulinzi na uwezeshaji. Kama vile Roho Mtakatifu alivyo Msaidizi wetu mkuu anayetuwezesha pale tunaposhindwa, ndivyo Mungu alivyomweka mwanamke kama mwezeshaji mkuu wa mwanamume ili kusudi la Mungu lifanikiwe. Mwanamume hajakamilika bila mwanamke, na mwanamke hajakamilika bila mwanamume; wote ni jeshi moja!
1. MWANAMKE SIO DHAIFU: Ukweli wa Ulimwengu wa Roho
Udhaifu ni mtazamo wa kimwili tu. Katika ulimwengu wa roho, mwanamke amebeba "hazina" inayomfanya awe mlengwa mkuu wa shambulio la adui. Shetani si mjinga; anapokuja kushambulia familia, anafanya utafiti wa "nani mwenye nguvu." Mara nyingi, anajua kuwa kama akimfunga mwanamke (mwenye neema ya uzazi wa kiroho na ushawishi), familia nzima itayumba.
Andiko la Kufundisha:
"Hata hivyo, hakuna mtu awezaye kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka mali zake, isipokuwa kwanza amemfunga yule mwenye nguvu; ndipo atakapoiteka nyumba hiyo." (Marko 3:27).
Shetani anapojaribu kuvunja ndoa au kuzuia huduma, mara nyingi huingiza hila zake kwa mwanamke kwanza kwa sababu anahofia nguvu ya maombezi na ushawishi wa mwanamke anayejitambua. Injili ya kwanza ya ufufuo ilihubiriwa na mwanamke (Yohana 20:16-18); Yesu alimwamini mwanamke kuwa mjumbe wa injili kuu. Hii ni ushahidi tosha kwamba mwanamke anayo "sauti" yenye mamlaka ya kubadilisha ulimwengu.
2. KUSUDI LA MUNGU: Mwanamke kama Msaidizi wa Kimkakati
Mwanamke si wa kuwekwa nyuma ya pazia, bali ni mshirika wa kutawala. Mungu alipowaumba, aliwapa agizo la pamoja:
"Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, 'Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale...'" (Mwanzo 1:28).
Kutawala si kazi ya mwanamume pekee. Mwanamke anapokuwa msaidizi, anafanya mambo yafuatayo:
Ongezeko la Huduma: Mwanamke ana "roho ya uzazi." Kile anachokigusa mwanamke aliyeokoka, huwa na baraka ya kuzaliana. Huduma nyingi zinazokua kwa kasi zina wanawake waliojitolea kuomba na kutumika kwa uaminifu.
Ulinzi wa Familia: Biblia inasema, "Mwanamke atamlinda mwanamume" (Yeremia 31:22). Mwanamke mwenye hekima hujenga nyumba yake (Mithali 14:1). Mke anapoomba, mumewe anapokea ulinzi wa kimalaika na neema ya wokovu.
Mshirika katika Uongozi: Mwanamume anaweza kuwa na maono, lakini mwanamke anatoa ule "ukamilifu" ili maono hayo yatimie.
3. WITO KWA WANAUME NA WATOTO: Thamini Msaada wa "Jeshi" Lako
Wanaume, tambueni thamani ya mama/mke wenu. Nyuma ya kila mwanamume anayesimama imara, kuna mwanamke anayelinda "mzunguko" wake kwa maombi na hekima. Mwanamke anapokuwa dhaifu au kuvunjika moyo, nyumba yote inakuwa katika hatari ya mashambulizi.
Vivyo hivyo, watoto lazima wajifunze kutambua nguvu ya mama zao. Mama si tu mlea, bali ni mlinzi wa kiroho wa nyumba. Shetani anawinda wanawake kwa sababu anajua uwezo wao wa kubadili historia ya familia. Mwanamke anapoamua kuwa "Komando," adui hana nafasi.
4. KUVUNJA DHANA POTOFU: Mama wa Nyumbani si "Mama Asiye na Kazi"
Moja ya silaha kuu za adui katika kuharibu thamani ya mwanamke ni kupandikiza dhana kwamba mwanamke anayehudumia familia yake nyumbani "hana kazi." Huu ni uongo mkubwa unaolenga kumvunjia mwanamke heshima na kumfanya ajihisi hafanyi chochote cha maana.
Ni lazima tuweke wazi: Kazi ya nyumbani ni KAZI kubwa, nzito, na ya msingi katika jamii. Mwanamume anapotoka nje na kurejea nyumbani, anasubiri kupokelewa na "pole" kutoka kwa mkewe kwa kazi aliyoifanya. Lakini je, ni nani humpa pole mwanamke ambaye tangu asubuhi amekuwa mlezi, mpishi, mwalimu wa watoto, msafi, meneja wa bajeti, na mshauri wa familia?
Kama mwanaume anajiona anafanya kazi kwa sababu anapata mshahara, mwanamke anafanya kazi ya "ujenzi wa taifa" kupitia malezi ya watoto na uimarishaji wa ustawi wa familia. Kazi anayofanya mwanamke ndani ya nyumba ni nguzo inayomfanya mwanaume aweze kwenda nje na kufanikiwa. Bila mwanamke huyu anayesimama imara nyumbani, msingi wa mwanaume ungeporomoka. Kwa hiyo, kumwita mama wa nyumbani "mama asiye na kazi" si tu ni ujinga, bali ni kutothamini nguvu na hekima inayojenga taifa.
Katika ulimwengu wa roho, mwanamke huyu ni "daktari wa nyumbani" na "mwangalizi mkuu." Hivyo, mwanaume anapaswa kutambua kuwa anapomwambia mke wake "pole" kwa kazi za nyumbani, hatendi fadhila, bali anatekeleza haki ya kumthamini mfanyakazi mwenzake katika ujenzi wa ufalme wa Mungu. Kazi ni kazi, iwe ya ofisini au ya nyumbani; zote zinahitaji hekima, nguvu, na kujitolea.
5. HITIMISHO: Simama Katika Nafasi Yako!
Mwanamke, wewe ni mlinda mlango wa ndoa yako na familia yako. Dunia na Kanisa vinakuhitaji kama daktari wa familia, mwalimu, na hakimu. Shetani anakuhofia kwa sababu anajua kile ulichonacho ndani yako ni kikuu kuliko mashambulizi yake.
Mwanamke mwenye hekima (anayejitambua) atasimama kwenye nafasi yake na kuhakikisha mumewe haanguki wala kufedheheka, huku akiing’arisha familia yake bila kusahau kuwa Kanisa linamuhitaji katika kuhakikisha adui hapati nafasi ya kuleta uharibifu.
Ushauri wa mwisho:
Jitambue: Unayo nguvu ya kipekee ambayo mwanaume hana.
Kua Kiroho: Huduma yako na maombezi yako ni ufunguo wa ushindi wa familia.
Kataa Kudharauliwa: Wewe si dhaifu; wewe ni mwezeshaji wa kusudi la Mungu.
Kama mwanamke ameokoka na kumaanisha, hata mume atapokea neema ya wokovu, na watoto watalindwa na Bwana. Shetani anajua kuwa duniani yupo mwanamke; sasa ni zamu yako kujijua!
Mada hii ni pana sana na ni ya msingi kwa ustawi wa familia zetu. Kwa sababu ya uzito wake, tutaendelea kuichambua kwa kina zaidi katika makala ijayo, ambapo tutaangalia namna mwanaume anavyoweza kuwa mshirika bora katika kumsaidia mkewe kutimiza wito huu, na jinsi familia inavyoweza kushinda mashambulizi ya giza kwa umoja. Usikose!
#MWANAMKE, Tunza Nafasi Yako na Jiamini Mahali Ulipo!
"The Woman is a Threat: Unlock your true identity to protect your family and rule with divine wisdom." _GDBxhop
Happy & Blessed All Women
Mtoto wa Mama, Gershom
✉️ Ministry: rhemaforlifeministry@gmail.com
✉️ Personal: gchallo30@gmail.com
🌐 Rhēma For Life Ministry

Comments
Post a Comment