Ni Roho wa Bwana Pekee Aumbaye Moyo Mpya: Siri ya Kudumu katika Mapenzi ya Kristo

 

Kiongozi anayemtegemea Mungu, ikiwakilisha uumbaji wa moyo mpya na roho mpya kupitia neema ya Kristo – GDeBh.
"Faith is not the absence of thorns, but the grace to walk above them." — GDeBh

NI ROHO WA BWANA PEKEE AUMBAYE MOYO MPYA: Siri ya Kudumu katika Mapenzi ya Kristo

Na: Mwl. Challo GC

"Nitawapa moyo mpya na kuweka roho mpya ndani yenu, nitaondoa ndani yenu moyo wenu wa jiwe na kuwapa moyo wa nyama." — Ezekieli 36:26

Utangulizi: Roho na Moyo kama Makao ya Utu

Katika safari ya imani, changamoto kubwa ambayo waamini wengi hukutana nayo si ukosefu wa dini, bali ni umaskini wa uwezo wa ndani wa kutenda mapenzi ya Mungu. Wengi hujaribu kubadilisha tabia zao, kuacha mazoea mabaya, na kutafuta utakatifu kwa kutegemea nguvu za utashi wao wenyewe (human willpower). Hata hivyo, Biblia inatufundisha ukweli mmoja mkuu: Mungu pekee ndiye atowaye Roho aletaye moyo mpya. Si kwa jitihada za kibinadamu, bali kwa neema yake pekee inayotufanya tuweze kushika na kutenda mapenzi yake.

Katika Biblia, maneno Roho (Ruach - Kiebrania, Pneuma - Kiyunani) na Moyo yanabeba maana pana ya utu wa ndani wa mwanadamu. Moyo ndilo "makao makuu" ya maisha yetu—hapo ndipo tunapofikiri, tunapopenda, na tunapojenga tabia zetu. Kama tunavyo viungo vya nje vya mwili, ndivyo ndani ya roho kuna "viungo" vya ndani vinavyoishi na kutenda kazi. Mungu anaposema na roho yako, anasema na mtu uliyekamilika.

1. Shughuli ya Mungu: Kuondoa Moyo wa Jiwe

Nabii Ezekieli alionyesha hali ya watu walioanguka katika dhambi na kujinajisi. Moyo wa mwanadamu ukiwa mbali na Mungu huwa kama jiwe: halihamishiki, halioni, na halisikii. Dhambi inapokolea, moyo huwa mzito na roho hufa. Hapa ndipo hitaji la Kuzaliwa Upya linapokuja.

Mungu hataki "kurekebisha" moyo wa jiwe kwa kuupaka rangi ya nje; anauondoa kabisa. Hii ni shughuli ya kiungu (Divine Operation). Mungu anatoa moyo wa nyama—moyo unaoweza kuhisi maumivu ya Mungu (huzuni ya Roho), kuelewa mapenzi yake, na kutii maelekezo yake kwa furaha. Huu ni moyo ambao unaguswa na Neno la Mungu badala ya kuwa na ukuta wa ukaidi.

2. Matokeo ya Kumpokea Roho wa Mungu

Unapompokea Yesu Kristo, Roho Mtakatifu haji tu kama mgeni anayetembelea, bali anakuja kama Muumbaji wa ndani (The Creative Spirit). Uwepo wake unaleta mabadiliko ya kimfumo:

Akili Mpya: Roho Mtakatifu anakuingizia hekima na busara za kiungu. Unaanza kuona maisha, changamoto, na watu kama Mungu anavyowaona.

Nafsi na Hisia Mpya: Unaanza kufurahia kile Mungu anachofurahia na kuchukia kile kinachomchukiza Mungu. Hii inaitwa utakaso wa hisia.

Uwezeshaji (Empowerment): Unapata nguvu ya kukwepa mauti na kufuata amri za Mungu. Unapokuwa na Roho wa Bwana, unakuwa "Ndani ya Roho," unakuwa "Mwenye Roho," na "Unaoongozwa na Roho." Hii ndiyo siri ya ushindi na utauwa katika ulimwengu huu wenye shinikizo kubwa.

3. Uwakili wa Kiroho: Kudumu katika Mapenzi ya Kristo

Kama Leadership & Stewardship Strategist, naona kuwa uaminifu wa kiongozi unategemea hali ya moyo wake. Kiongozi mwenye moyo wa jiwe hawezi kuwa msimamizi mwaminifu; atatafuta faida zake binafsi. Lakini kiongozi mwenye moyo wa nyama (moyo wa Roho) anaelewa kuwa yeye ni wakili tu.

Ukimya, nidhamu, na ujasiri wa kusonga mbele vinatokana na Roho anayekaa ndani yetu. Tunapokuwa na Roho wa Bwana, uongozi wetu haujengwi kwa kelele, bali kwa matunda ya Roho. Tunapopitia majaribu, hatuyumbishwi kwa sababu msingi wetu wa ndani umeshabadilishwa na Roho wa Mungu.

Hitimisho

Mpendwa, moyo mpya ni moyo akaao Roho Mtakatifu. Unapoondoa moyo wa kale, yale yote maovu ya kale huondoka na unakuwa huru kuzifurahia baraka za Mungu katika nchi yako. Usitegemee nguvu zako; mkaribishe Roho wa Mungu afanye kazi ya uumbaji ndani ya moyo wako leo.

Sala Fupi:

Ee Bwana, tunakushukuru kwa Neno lako. Tunakuomba utusaidie kuzielekeza nia zetu katika kusikiliza, kushika, na kutenda unayotuamuru. Ondoa roho ya uasi ndani yetu na utupe moyo wa utii wa hiyari, ili tuwe tunu machoni pako. Katika jina la Yesu, Amina.

"Obedience is not a price you pay, but a protection you receive from God." — GDeBh

Mwl. Challo GC

Leadership & Stewardship Strategist


Cat. Gershom E. Challo
Developing Excellence & Building Holistically
Rhēma For Life Ministry
Driven-Stewardship, Transforming Lives
Ethical Stewardship | Leadership | Spiritual Growth
#GDeBh | #ChalloFamilyLibrary

Comments

Popular posts from this blog

Ndoa: Heshima, Usafi & Hukumu

Uongozi kama Wito, Sio Cheo

Wokovu Mara Moja: Utimilifu wa Neema katika Maisha ya Mwamini